JESHI la Polisi mkoani Kagera linawashikilia watu tisa kwa tuhuma za mauaji katika matukio mawili tofauti wakiwemo mume na mke waliomuua mganga wa jadi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani hapa Henry Mwaibambe, alisema tukio la kwanza lilitokea saa 3:00 usiku wa Januari 14 mwaka huu katika kata ya Bugarama wilayani Ngara ambapo mganga wa jadi, Alfaxad John ( 36 ) akiwa anaendesha pikipiki yake yenye namba za usajili T.237 CDK alikufa baada ya kupigwa na kitu chenye ncha kali.
Alisema inaaminika mganga huyo alipigwa na shoka kichwani na kusababisha kichwa kugawanyika sehemu mbili na shingo kutenganishwa.
Alisema siku mbili kabla ya tukio hilo la mauaji John aliibiwa mbuzi watano nyumbani kwake, aliwaona wezi lakini hakutoka nje ili kulinda usalama wake.
Baada ya muda alipata ujumbe wa simu ya mkononi kutoka kwa mpenzi wake ukisema “pole mpenzi nipo pamoja na wewe ungetoka nje ili kukabiliana na wezi hao ungeuawa”.
Aliwataja watuhumiwa wanaoshikiliwa kuwa ni Burhani Tutuleka (40 ) mwalimu wa shule ya msingi Rwinyana iliyoko kata ya Bugarama na mkewe Madina Khamisi (35).
Ingawa chanzo cha mauaji hayo bado hakijajulikana lakini mke wa mtuhumiwa alikuwa anatibiwa na John na mumewe alikuwa akimtuhumu mganga huyo kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na mke wake.
Kamanda Mwaibambe alisema tukio la pili lilitokea saa 8:30 usiku wa Januari 15 mwaka huu ambapo kundi la wahalifu wasiopungua 10 walimvamia na kumuua Onesmo Mutta ( 24 ) mkazi wa Mtaa wa Katotorwansi kata ya Kashai Manispaa ya Bukoba.
Alisema katika tukio hilo wahalifu hao walivamia nyumba aliyokuwa akiishi Mutta ambayo ilikuwa na wapangaji wengine na kuanza kuwapiga na kudai kupatiwa fedha huku wakiwa wamebeba mapanga na marungu.
Alisema Mutta alichomwa na kitu chenye ncha kali kifuani upande wa kushoto na kufa papo hapo. Alisema wapangaji wengine watatu na mke wa Mutta walijeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao.
Wahalifu hao walifanikiwa kuiba vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh 400,000. Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Philipina Onesmo mke wa Mutta ,Edwin Haipolite (23 ) mjasiriamali, Adelene Simon (27 )n a Denice Gervas.
No comments:
Post a Comment