Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na vijana lijulikanalo kama Restless Development, Joseph Bukula, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi wa upimaji afya kwa hiari uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Bukula alisema vijana wanachotakiwa kufanya kwa wakati huu ni kuhakikisha kuwa wanajitambua kwa kufanya kile kilicho wapeleka chuoni na si kujiingiza katika biashara zisizofaa na zinazoshusha maadili yao.
Alibainisha kuwa vijana wengi hasa waliopo katika vyuo mbalimbali wamekuwa wakiingia katika mitego inayowapelekea kujikuta wakipata maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutokana na wao kushindwa kujitambua.
"Kijana kama atajitambua anaweza kufanya mambo yake bila hofu yoyote pia haitakuwa rahisi kwa yeye kudanganyika kwani kujitambua kwake kutamjengea kujiamini," alisema Bukula.
Aidha alisema bado kuna changamoto kubwa ya elimu kwa vijana juu ya masuala ya upimaji Ukimwi kwa hiari kutokana na kutokwepo kwa idadi kubwa ya watu wanaojitokeza.
Alisema lengo la kuendesha zoezi hilo la upimaji katika chuo hicho ni kuwasaidia vijana kutambua afya zao pia kupata elimu ya maambukizi hayo na kuweza kujikinga.
"Restless inatoa elimu kwa vijana juu ya ugonjwa wa Ukimwi kwa vijana wa chuo hiki lakini ambapo pia tumezindua bango chuoni hapa lenye ujumbe kwa jamii linalosema eneza elimu na si virusi," alisema Bukula.
Naye Mratibu wa miradi wa shirika hilo Selestine Ngowi, alisema kuwa mradi huo wa kutoa elimu kwa vijana utakuwa endelevu ili kuweza kuwasaidia vijana walioko chuoni na mitaani kuweza kujikinga na virusi vya Ukimwi.
No comments:
Post a Comment