Wednesday, January 21, 2015

MWENYEKITI WA KITOGOJI AUZA ENEO LA KIJIJI EKARI 200 KWA SHILINGI MILIONI 6 Wananchi wadai Ardhi Yao


Siku chache baada ya kuchaguliwa na wananchi na kuapishwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sabasita kijiji Hihumbu kata ya Unyali wilaya ya Bunda Joseph Kitosha, anadaiwa kuuza eneo lilotengwa na kijiji kwa ajili ya wafugaji zaidi ya ekari 200 kwa shilingi Milioni 6.

Wananchi wa eneo hilo wanadai kuwa wakati wa uongozi uliopita Serikali iliwatengea eneo hilo la ekari 200 wafugaji hao kwa ajili ya malishio ya mifugo yao hapo kijijini.
Katika mkutano uliofanyika kijijini hapo chini ya Mwenyekiti wa wafugaji kanda ya ziwa Mulida Mushota, wafugaji hao walieleza kuwa mwenyekiti wa kitongoji hicho alishirikiana na Mtendaji wa kijiji  na kuuza eneo hilo kwa mwekezaji.

Walibainisha kuwa eneo hilo ambalo ni tegemeo kubwa sana kwao, kwa ajili ya kulishia mifugo yao, limeuzwa kinyume cha utaratibu bila ya kushirikisha wananchi, huku wakidai kuwa mwenyekiti huyo alipewa kiasi cha shilingi  laki mbili ili kuruhusu uuzaji wa eneo hilo.

“..huu ni wizi wa hadharani mwekekiti tumemchagua hata mwezi haujafika…jambo la kwanza ameanza kuuza eneo letu hii ni hajabu sana ..eneo hilo likienda kwa mwekezaji mifugo yetu tunaipeleka wapi? tutakuwa wageni wa nani? Hatukubali hata kidogo eneo letu liende hivihivi” Alisema Uchai Mnada

Wananchi walienda mbele zaidi kwa kuitaka ofisi ya Mkuu wa Wilaya Bunda kuingilia kati sakata hilo, huku wakidai kuwa ikiwa eneo lao litachukuliwa wao watapambana ili kupata haki yao hata ikiwa kwa vita.




“…hatukubaliana hata kidogo eneo letu kuchukuliwa na wajanja, tumechoka sasa wafugaji maeneo yetu kuchukuliwa kila mara…hapa tutapamba na hata kwa vita tutafika ikishindikana kutatuliwa na serikali, tutaenda mahakamani lakini na uko ikishindikana tutapambana kwa nguvu zetu” Alisema Sucha Bule.

Alipotakiwa kutoa maelezo mbele ya Mkutano huo Mwenyekiti huyo alikiri kuhusika kuuza eneo hilo, huku akieleza kuwa alielezwa kuwa eneo hilo ni mali ya wanakijiji aliowataja Pilli Mnada pamoja na Sucha Bule.

Alisema kuwa wananchi hao ambao wanaishi ndani ya kitongoji hicho siku ya kufanyika mauzo walionyesha hati za umiliki wa eneo hilo, hali aliyoeleza ilimfanya kukubali na kuweka sahihi katika mkataba wa kuuzwa kwa eneo hilo.

  wakati wa kuuzwa kwa eneo hilo hawa wanakijiji tena wanaishi hapa ndani ya kitongoji changu..walionyesha hati za umiliki wa eneo hilo..na mimi niliitwa na mtendaji wa kijiji kuwa shahidi katika mauziano hayo..nilipoona hati nikakubali sikuwa na kipingamizi lakini suala la kupewa rushwa siyo kweli” Alisema Katosha amabaye ni mwenyekiti wa eneo hilo.

Hata hivyo maelezo hayo yalikataliwa na wananchi na kutaka kumpiga katika mkutano huo, ambapo aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji kabla ya uchaguzi kufanyika Tomasi Kiteta alisema madai ya mwenyekiti huyo siyo kweli.

Alisema wakati wa uongozi wake akiwa mwenyekiti wa kijiji eneo hilo walilitenga kwa ajili ya malisho ya ng’ombe wa wafugaji huku akidai kuwepo kwa mtahasari wa kutengwa eneo hilo ulipitishwa na serikali ya kijiji.

Kwa upande wake Mwenyekiti huyo wa wafugaji kanda ya ziwa aliitaka ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na TAKUKURU kufaya uchunguzi juu ya jambo hilo ikiwa pamoja na kuwachukuliwa hatua za kisheria wahusika wote.

“ kijiji hiki kina mifugo wengi sana..na hili eneo likiuzwa wafugaji wetu wataangaika sana na mapigano yataongezeka, tunaiomba TAKUKURU waje wafanya uchunguzi lakini Mkuu wa wilaya na yeye achukue nafasi yake kuwawajibisha watendaji wake kama hawa” Alisema Mushota.

Hata hivyo wananchi hao waliunda kamati ya watu 5 kwa ajili ya kufuatilia jambo hilo, katika ofisi ya Mkuu wa wilaya ikiwa pamoja na kwenda mahakamani kupinga uuzwaji wa eneo lao.

CHANZO: SIMIYU NEWS

No comments:

Post a Comment