OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imetoa siku nane kwa Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Augustino Mrema kutoa maelezo kuhusu tuhuma za kuendesha chama hicho kinyume na katiba.
Hayo yalibainishwa juzi katika taarifa iliyotolewa Dar es Salaam na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza ambayo ilimtaka kuwasilisha maelezo yake kabla ya Januari 23, mwaka huu ili ofisi hiyo iweze kuyafanyia kazi na kuwajibu walalamikaji.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukweli na Maridhiano TLP Taifa, Joram Kinanda, pamoja na Mrema kukiuka katiba ya chama chao, pia anatuhumiwa kuongoza chama kidikteta, kujilimbikizia madaraka na kuporomosha heshima ya chama cha upinzani.
Kinanda aliongeza kuwa Mwenyekiti huyo, anaendesha chama hicho kwa ukabila kitu ambacho ni tofauti na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 na ni tofauti na katiba ya chama chao.
Hata hivyo katika barua yake kwa Msajili, Kinanda aliiomba ofisi hiyo ifanyie kazi tuhuma hizo na kuruhusu Kamati ya Ukweli na Maridhiano kutambuliwa na kupewa mamlaka ya kuongoza TLP kuelekea uchaguzi mkuu.
Pia aliomba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itangaze kwamba Uongozi wa Mrema umekoma.
Akifafanua kuhusu hatua hiyo, Nyahoza alisema kwa mujibu wa kanuni ya 13 ya kanuni za usajili wa vyama vya siasa mlalamikiwa huyo atatakiwa kuwasilisha majibu ya tuhuma hizo kwenye ofisi yake siku iliyopangwa na sio zaidi ya hapo.
No comments:
Post a Comment