Wednesday, January 21, 2015

Kama Unataka Kuwa Na Mafanikio Makubwa Mwaka 2015, Acha kufanya Mambo Haya.

Kujenga mafanikio makubwa unayoyataka ni kitu cha muhimu sana katika maisha yako. Maisha haya ya mafanikio tunayozungumzia huwa hayaji tu kwa bahati mbaya, huwa yanakuja kwa kujiwekea mipango na malengo, kujitoa kwenye mafanikio na kufanya kila linalowezekana, lakini wakati mwingine maisha haya ya mafanikio huwa yanakuja kwa kuwa na nidhamu binafsi itakayokuongoza kujizuia kufanyamambo ya aina fulani ambayo umekuwa ukiyafanya na kukuzuia kweye mafanikio.

Pamoja na wengi  kutambua umuhimu wa kufikia mafanikio makubwa wanayotaka. Hata hivyo, kwa muda sasa imekuwa ngumu kufikia mafanikio hayo kutokana na kufanya mambo ambayo hayaendani na ndoto zao. Najua umekuwa una kiu na shaku kubwa ya kutaka kuachana na maisha unayoishi sasa na umekuwa ukitamani uwe na maisha mengine mbayo utaishi kwa kuyafurahia hasa mwaka huu wa 2015. Kama kweli unataka kuwa na mafanikio makubwa mwaka 2015, acha kufanya mambo haya:-

1. Acha kuwa na kisirani kwa wengine. 
Hili ni jambo ambalo unalotakiwa kuwa nalo makini katika safari yako ya mafanikio. Acha kuwa na kinyongo na kuwaonea wivu sana watu wengine wengine waliofanikiwa zaidi yako. Ikiwa utakuwa unaishi maisha haya ya kuwa na kinyongo hutafanikiwa sana. Hii ni kwa sababu utakuwa unatumia nguvu nyingi kijihami na matokeo yake utashindwa kujifunza vitu vya msingi ambavyo vingekusaidia hata wewe kufanikiwa. Hata kama waliofanikiwa ni adui zako jifunze kitu kwao na kisha chukua jukumu la wewe kubadilika.

2. Acha kuangalia nyuma. 
Katika safari yako ya mafanikio jifunze kutokuangalia nyuma, hata kama ikitokea mambo kwako yamekuwa magumu vipi. Usijalaumu wala usijute kwa kufikiri kuwa pengine kuna sehemu ulikosea na kutamani kurudi nyuma ama kuacha kile unachokifanya. Jifunze kutafuta njia mpya itakayokuwezesha kuruka vizuizi vilivyoko mbele yako na sio kusimama na kuanza kutamani kuangalia nyuma. Kama utazidi kuangalia nyuma na kushindwa kuchukua hatua za kusonga mbele, sahau mafanikio katika maisha yako.

3. Acha kutafuta visingizio kila mara. 
Kuna ambapo hasa pale mambo yako yanapokwama huwa unajikuta ni mtu wa kutafuta visingizio hiki na kile. Kama mambo yako yamekwenda tofauti na ulivyotarajia acha kutafuta visingizio, badala yake tafuta chanzo cha tatizo la mambo yako kwenda vibaya. Na kama utagundua chanzo cha tatizo lako hautatafanya kosa hilo kwa mara nyingine tena na utajikuta utakuwa umegundua mzizi wa tatizo linalokusumbua na utaacha visingizio. Kuwa ni visingizio ni kitu kikubwa kinachokuzuia kutofikia ndoto zako kubwa ulizojiwekea.

4. Acha kusimama kujifunza. 
Hili ni jambo ambalo tumekuwa tukilizungumza na kulitilia msisitizo mara kwa mara katika mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kuwa, ili uweze kufanikiwa na kufikia mafanikio unayoyataka ni muhimu kwako kujifunza kila siku. Hakuna kitu kinachokuzuia wewe kujifunza kila siku na kufikia mafanikio makubwa unayotaka. Jenga tabia ya kujifunza kila siku, wala usichoke,  utajikuta  ukigundua vitu vingi sana ambavyo ingekuwa sio rahisi kama ungekaa tu na kupoteza muda wako bila sababu. Kama unataka mafanikio makubwa, anza kujifunza sasa.


5. Acha kuwa na watu hasi katika maisha yako. 
Kama utakuwa unaishi na kuzungukwa na watu wanaolaumu tu, walalamikaji, wapondaji na wakosoaji wakubwa wa mambo ya wengine, elewa upo kwenye hatari ya kutokufanikiwa kwa asilimia mia moja. Watu hawa ni hatari sana kwenye maisha yako kwa sababu watakuwa wananyonya nguvu zako, bila mwenyewe kujijua na mwisho wa siku utajikuta na wewe unaishi maisha hayohayo ya kulaumu na kuponda wengine. Umefika wakati wa wewe kuamua na kuachana na watu hawa, maana kwa vyovyote vile watakurudisha nyuma.


6. Acha kuishi maisha ya kushindwa kuipangilia siku mapema. 
Kama utakuwa unaishi maisha ya kutoipangilia siku yako mapema, ama kutoweka mipango yako vizuri kwa siku inayofuta utajikuta utakuwa ni mtu wa kupoteza muda tu kila mara. Kuweza kufanikisha hili ni muhimu kwako wewe kujiwekea malengo au ratiba ambayo utakayokuwa ukiifuata na kuitekeleza ili kuepuka kupoteza muda kwa mambo ambayo siyo ya msingi. Ukiweza kufanya hivyo utakuwa unajijengea tabia bora itakayokuongoza kwenye mafanikio. Kuipangilia siku mapema ni muhimu sana kwa mafanikio yako.

7. Acha kuwa mwongeaji sana wa ndoto zako.
Kama umekuwa ukiongelea sana ndoto zako na umekuwa ukichelewa kutekeleza mipango yako ni wakati wa kuachana na hiyo hali sasa. Watu wenye mafanikio huwa ni watu ambao sio waongeaji sana juu ya ndoto zao. Huwa ni watu wa mipango na malengo kisha kutekeleza kile walichokipanga. Kama utaendelea kuongea na kuongea tena juu ya ndoto zako, elewa kabisa hutafanikisha kitu na utaendelea kuishi maisha yaleyale magumu. Kama unataka kubadili maisha yako, acha tabia hii ya kuongelea ndoto zako kuwa mtu wa vitendo.
 SOMA: Hivi ndivyo unavyofanya maisha yako kuwa magumu zaidi.

Kwa vyovyote vile iwavyo, tabia, mienendo uliyonayo katika maisha yako ina uwezo mkubwa wa kuathiri maisha uliyonayo. Chukua hatua sahihi na jukumu la kukubali kuwajibika kubali maisha yako na kukataa kwa nguvu zote mambo yote yanayokuzuia wewe kufikia mafanikio katika maisha yako. Kama una nia ya kweli kubadili maisha yako, achana na mambo hayo, mafanikio makubwa yatakuwa upande wako siku zote na hilo linawezekana.

Nakutakia mafanikio mema, karibu sana katika KISIMA CHA MAARIFA kujifunza mambo mazuri ya mafanikio.

Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuhamasika zaidi.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,
0767 048 035/dirayamafanikio.blogspot.com
0713 048 035/ingwangwalu @gmail.com

No comments:

Post a Comment