Sunday, January 18, 2015

Nyotamkia ya uzito wa tani 12,kivutio kikubwa cha watalii huko Mbeya



MOJA ya vivutio adimu vya utalii vinavyowashangaza wengi wa watalii wa ndani na nje wanaotembelea Mkoa wa Mbeya, ni nyotamkia (kimondo) inayopatikana katika Kijiji cha Ndolezi, Wilaya ya Mbozi. Wenyeji wa mkoa huo, wanasema nyotamkia hiyo ilianguka mahali hapo mwaka 1840.
 
Kila siku, hasa za Jumamosi na Jumapili, idadi kubwa ya watu husafiri kutoka sehemu mbalimbali nchini na duniani kwa ujumla, hadi katika kijiji cha Ndolezi kw ajili tu ya kuangalia maajabu ya nyotamkia hiyo, inayodaiwa kuchomoka kutoka katika njia yake (orbit) iliyoko anga za mbali na kisha kuangukia kijijini hapo.
 
Kwa mujibu wa maelezo ya wasimamizi wa kivutio hicho cha utalii kwa FikraPevu, nyotamkia hiyo ina uzito wa takriban tani 12, ikiwa ni ya nane kwa ukubwa duniani kati ya nyotamkia zaidi ya 600 zilizoanguka kutoka angani sehemu mbalimbali ulimwenguni. Inaelezwa kuwa nyotamkia hiyo ya Kijiji cha Ndolezi, inaongoza kwa ubora ikilinganishwa na nyotamkia zilizoanguka sehemu mbalimbali ulimwenguni. Aidha, nyotamkia hiyo, au kimondo kama kinavyofahamika kwa wengi, kinaelezwa kuwa na madini ya chuma kwa zaidi ya asilimia 90.

 
Hakuna maelezo ya mtu yeyote katika eneo hilo anayedai kushuhudia wakati nyotamkia hiyo ikianguka mahali hapo mwaka 1840, bali maelezo yaliyopo ni kwamba iligunduliwa kuwepo hapo ilipo wakati wa utawala wa Mjerumani mwaka 1930, ambapo mwaka 1931, watalaamu wa nyota hizo wa Kijerumani, walikata kipande cha nyotamkia hiyo na kukipeleka nchini mwao kwa ajili ya kukifanyia utafiti na uchunguzi zaidi.
 
Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa, Philipo Maligissu, katika kuelea nyotamkia hiyo, anasema baada ya wataalam hao wa Kijerumani kuipima ilibainika kuwa na urefu wa mita tatu, unene wa mita 1.12, upana mita moja na uzito wa tani 12. Mbali na kuwa na madini ya chuma kwa zaidi ya asilimia 90, nyotamkia hiyo inaelezwa kuwa na na aina nyingine nne za madini yanayounda asilimia chini ya 10 inayobaki.
 Mhifadhi Kiongozi huyo wa Makumbusho ya Taifa, Maligissu, anasema kwa hapa nchini, hadi sasa kuna nyotamkia nane zilizoanguka katika maeneo mbalimbali. Baadhi ya nyotamkia hizo ni pamoja na Lichinga iliyoko mkoani Mtwara, yenye uzito wa chini ya kilo. Nyotamkia hiyo, inadaiwa kuonwa na baadhi ya wananchi wa eneo hilo wakati inaanguka mwaka 1949.
 
Nyingine inapatikana wilayani Mbulu, Mkoa wa Manyara ambayo haikuonekana wakati ikianguka kutoka angani, nyotamkia ndogo iliyoko katika Kijiji cha Ivuna, wilayani Mbozi inayodaiwa kuonekana wakati inaanguka hapo mwaka 1938, nyotamkia ya Malampaka, Mkoa wa Shinyanga ambayo ilionekana kwa macho wakati inaanguka mwaka 1930, nyotamkia ya kijiji cha Litowa, Peramiho, mkoani Ruvuma ambayo katika historia ya nchi hii ndiyo ya kwanza kuonekana kwa macho wakati inaanguka mwaka 1899.
 
kwa mujibu wa ‘Abate’ Mstaafu wa Peramiho, Mhashamu Lambert Doerr OSB (80), nyotamkia hiyo ya Litowa ilionekana kwa baadhi ya wananchi wa eneo hilo wakati inaanguka kutoka angani, ingawa ilikuwa ndogo sana, lakini wamisionari wa Kijerumani wakati huo waliwafahamisha wenyeji kwamba hiyo ni nyotamkia, wasigope.
 
“Nyotamkia ya Ndolezi Mbozi ni kitega uchumi adimu cha utalii kwa kuwa watalii wengi wanasafiri na kuja hapa ili kuona maajabu ya vitu ambavyo vimemeguka kutoka sayari nyingine katika anga za mbali na kushuka kama nyota hadi katika dunia tunayoishi. Wengi watalii hao wanapenda kujifunza vitu ambavyo havipatikani katika dunia tunayoishi,” anasisitiza Maligissu.
 
Hata hivyo, mtaalamu huyo wa mambo ya kale anasema jamii inatakiwa kufahamu kwamba nyotamkia hiyo ya mkoani Mbeya ni hazina kubwa na ya kipekee ambayo inatakiwa kulindwa na kuendelezwa kwa kuwa watu wengi wanapenda kufika kujifunza  kielimu na kisayansi, na hivyo taifa kupata fedha za kigeni na kuongeza mapato.
 
Kwa mujibu wa mtaalam huyo, eneo ambalo nyotamkia imeangukia likiendelezwa linaweza kuwa chanzo cha kupunguza umasikini wa kipato kwa kuwa watalii wanapotembelea wanalipa kiingilio, wanalipia chakula ambacho kinauzwa na wenyeji kwa watalii, na wanalipia usafiri pamoja na kununua vifaa mbalimbali vya kiutamaduni kama vile vinyago na vifaa vingine vya asili ambavyo vinaweza kuuzika kwa watalii hao.
 
Uchunguzi ambao umefanywa katika Kijiji hicho cha Ndolezi chenye eneo ambalo nyotamkia hiyo ilianguka, umebaini kuwa kivutio hicho licha ya kuwa ni adimu na cha kipekee nchini, hakuna jitihada za makusudi zinazofanywa katika kukitangaza na kukiendeleza ili kuvutia idadi kubwa ya watalii wa ndani na nje kwa leng la kuinua kipato kwa wananchi na taifa.
 
Keneth Mwazembe, ni mwanaharakati wa utalii katika Wilaya ya Mbozi. Katika kuzungumzia kivutio hicho cha utalii, anasema licha ya nyotamkia hiyo kuanguka kwa miaka mingi katika Kijiji hicho cha Ndolezi, Idara ya Mambo ya Kale imeshindwa kuiendeleza ili iweze kuingiza mapato mengi kulingana na thamani ya nyota hiyo kiulimwengu.
 
“Kwa kweli nyota hii licha ya kuwa na sifa nyingi, mahali ilipoangukia pako wazi mno, hapajaendelezwa kwa kujengewa uzio, hivyo mtu yeyote akipita barabarani anaiona hivyo haoni haja ya kutoa ada ya kiingilio,” anasema Mwazembe na kuongeza: “Kama nyotamkia hii ingeendelezwa pamoja na eneo lenyewe kuboreshwa kwa kujenga hoteli na vivutio vingine, kwa kweli Serikali imepata kitega uchumi muhimu sana katika sekta ya utalii.”
 
Kwa upande wake, Mhifadhi Msaidizi wa Idara ya Mambo ya Kale, Filmerick Bassange, anasema licha ya nyotamkia hiyo kukabiliwa na changamoto mbalimbali, Serikali imeweza kuchukua hatua kadhaa, zikiwemo za kuiingiza nyota hiyo kwenye sheria ya mambo ya kale mwaka 1964, hivyo kuitambua na kutoa ulinzi ili isiendelee kuhujumiwa.
 
Basange anabainisha zaidi kuwa mwaka 1967, Serikali ya Tanzania iliamua kuchimba eneo ambalo nyota hiyo ilianguka na kujengea msingi ambapo kabla ya hapo nyota hiyo ilikuwa inaonekana sehemu ndogo ya juu kutokana na robo tatu ya nyota hiyo kuzama ardhini wakati inaanguka kutoka angani.
 
Gilbert Twente, miongoni mwa Wataalam Wahifadhi wa Mambo ya Kale. Anasema idadi kubwa ya watalii wa ndani wanaoongoza kwa kutembelea nyota hiyo, ni wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya juu wanaofika hapo kwa lengo la kujifunza kwa vitendo mada za sayansi inayohusiana na elimu ya anga.
 
“idadi watalii kutoka nje ya nchi bado ni ndogo ikilinganishwa na sifa za nyota hiyo. Hali hiyo inatokana na eneo hili kutotangazwa kiasi cha kutosha katika vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa. Matangazo yanaweza kuongeza idadi ya watalii kila mwaka, na hasa watalii wan je,” anasema Twente.
 
John Mgalla ni mmoja wa wazee katika eneo la Mlowo, wilayani Mbozi. Anasema kwa kiasi kikubwa eneo hilo limetelekezwa kiasi cha ubora wake kuanza kupungua kutokana na kukosa matunzo yanayostahili. Ametoa wito maalum kwa Serikali kuhakikisha kuwa inakiangalia kivutio hicho kwa macho yake yote ili kukitangaza na kuboresha miundombinu ili kuvutia watalii na wawekezaji.
 
Hata hivyo, Idara ya Mambo ya Kale kwa kushirikiana na Idara ya Makumbusho ya Taifa, chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii  zina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa Malikale zilizopo nchini, ikiwemo nyotamkia hiyo ya mkoani Mbeya, zinahifadhiwa, kulindwa na kuendelezwa, kwa kuwa ni urithi wa taifa kwa kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
 
Maligissu ameiambia FikraPevu aina ya madini, kiasi cha asilimia kilichomo katika nyotamkia hiyo kikiwa kwenye mabano, kuwa ni chuma (90.45), nikeli (8.66), shaba (0.69), sulfa (0.11) na fosiforasi (0.11).
 
“Inaaminika kuwa nyotamkia ya Mbozi ndiyo ya kwanza kwa ubora duniani ikilinganishwa na nyotamkia nyingine zilizoanguka ulimwenguni ambazo asilimia kubwa ni mawe, yakiwa uzito wa kuanzia kilo tano tu,” anasema Maligissu.
 
Utafiti uliopo unaonyesha kwamba nyotamkia hiyo ya mkoani Mbeya ndiyo pekee yenye aina tano hizo za madini, ikilinganishwa na nyotamkia nyingine ambazo zimekia kuwa mfano wa jiwe, ikiwemo nyotamkia inayoongoza kwa uzito ulimwnguni inayopatikana nchini Afrika Kusini yenye uzito wa tani 60, na ya pili iliyoko nchini Uingereza yenye uzito wa tani 30.

No comments:

Post a Comment