Friday, January 16, 2015

Binti acharazwa fimbo 15 makalioni kisa mchango wa mlinzi wa shule

Mwanafunzi wa kike wa Shule ya Msingi Nsalaga Kata ya Nsalaga Uyole anayesoma Darasa la saba jina linahifadhiwa amecharazwa fimbo 15 sehemu mbalimbali za mwili wake na Mwalimu wa Darasa baada ya kushindwa kuakilisha mchango wa Mlinzi wa shule hiyo.
Tukio hilo limetokea shuleni hapo mapema Januari 6 mwaka huu baada ya kufunguliwa shule hiyo ambapo Mwalimu Abdon Mgina bila huruma alimcharaza fimbo 15 bila huruma na kumsababishia maumivu makali yalipelekea Mwanafunzi huyo kukimbizwa katika Hospitali ya Igawilo Jijini Mbeya.
Baada ya kurejea nyumbani Mwanafunzi huyo hali yake ilikuwa mbaya hivyo mama Mzazi aliyejitambulisha kwa jina la Elizabeth Enock (39) aliomba msaada kwa mtoa huduma majumbani Kata ya Nsalaga anayefahamika kwa jina la Ernest Nguku ambapo alipofika nyumbani kwa Mzazi wa mtoto alimshauri aende kutibiwa Hospitali.
Mapema Januari 7 mtoto alipelekwa Kituo cha Polisi Uyole ambapo alipewa PF 3 na kupatiwa matibabu katika kituo cha Afya Igawilo ambapo alitibiwa na kutakiwa kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara huku mtoto huyo akishindwa kuhudhuria masomo kutokana na maumivu makali.
Wakati wa tukio hilo Baba Mzazi wa Mtoto huyo Ahmed Shaban Kilanga(49) alikuwa hayupo nyumbani na aliungana na Mkewe kuendelea kumtibu Mwanafunzi huyo licha ya mazingira magumu waliyo nayo wazazi hao.
Baada ya kuona suala hilo limetolewa taarifa Polisi Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Daniel Mwamasangula kwa kushirikiana na Polisi waliamua kufanya kituo cha Polisi kama Mahakama na kumwamuru Mwalimu Abdon Mgina kumlipa Baba wa mtoto shilingi elfu thelathini kama fidia ya matibabu.
Uchunguzi wa awali umebaini PF 3 kutojazwa kikamilifu na Askari wa Kituo cha Polisi Uyole kwa nia ya kuficha uovu uliotendwa na mwalimu Abdon bila kujali Afya ya Mtoto.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Mussa Zungiza alisema hakubalianni na kitendo cha Mwalimu kumchapa mtoto badala yake angeitwa Mzazi ili awajibishwe kisheria badala ya kumwadhibu mtoto asiye na hatia.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nsalaga Timoth Mandondo Mwanamasanja amekiri kupokea malamiko ya suala hilo na kwamba ataonana na Kamati ya shule hiyo ili kulipatia ufumbuzi wa haraka ufumbuzi wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi amekiri kupokea taarifa za tukio hilo na kwamba baada ya kuwaita Wazazi wa mtoto huyo ofisini kwake Wazazi wameshidwa kutoa ushirikiano ili mwalimu afikishwe mahakamani ili ajibu tuhuma zinazomkabili lakini Wazazi wameshindwa kuonesha ushirikiano kwa kukataa kuchukuliwa hatua za kisheria Mwalimu aliyehusika na tukio hilo.
Baadhi ya Asasi zimekuwa zikipinga vitendo vya kikatili Mkoani Mbeya lakini bado vitendo hivyo vimekuwa vikishamiri siku hadi siku hasa lawama kubwa zikielekezwa katika vituo vya Polisi kwa kutosimamia sheria na baadhi kushidwa kutumia ueledi wa kazi zao.
Hivi karibuni Shirika la UNESCO liliendesha semina ya kutetea haki za watoto iliyofanyika ukumbi wa JM ili kuzipitia sheria mpya za sheria ya mtoto ya mwaka 2009,semina iliyoshirikisha Jeshi la Polisi,Mahakama,Sheria,Shirika la msada wa Kisheria na Taasisi ya Haki za Binadamu.
Maswali ya kujiuliza je anayepaswa kudaiwa michango mbalimbali ya shule ni mwanafunzi au mzazi?,na Vituo vya Polisi vimegeuka Mahakama au Mabaraza ya Kata na usuluhishi.
Mbali ya Wazazi kulalamikia michango isiyoeleweka katika shule hiyo lakini watoto wamekuwa wakichangishwa fedha za malipo ya masomo ya ziada(TUITION)kila Jumamosi kwa kulipa shilingi mia mbili lakini Kamati ya shule hajachukua hatua kukomesha michango hiyo na wakati mwingine watoto kutumiwa kuosha gari la mwalimu aina ya SUZUKI lenye namba T 477 ANT muda wa masomo.

No comments:

Post a Comment