Wakati Msajili wa Hazina amebariki posho mpya za safari za ndani kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) kuwa Sh 500,000 kwa siku kuanzia Januari 2, mwaka huu, imebainika kuwa walishaanza kulipana hivyo tangu mwaka 2011.
Hayo yalibainika wakati wa Kamati ya Bunge Hesabu za Serikari (PAC), ilipokutana na Menejimenti ya TPA jijini Dar es Salaam.
Kutokana na kamati hiyo kubaini posho hizo, zilianza kutumika hata kabla ya kupitishwa, imeiagiza Menejimenti ya TPA kuhakikisha wafanyakazi wote waliolipwa viwango vipya vya malipo ya safari kabla ya kuruhusiwa na Msajili wa Hazina wanazirejesha.
Agizo hilo la kurejeshwa kwa fedha za posho, limetolewa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, aliyesisitiza kuwa ni makosa kwa taasisi kuanza kutumia viwango vipya vya safari kabla ya kupewa kibali na Msajili wa Hazina.
Aidha, PAC imemuagiza Msajili wa Hazina kuhakikisha anafanya ukaguzi wa haraka kuangalia kama viwango kwa ajili ya safari vikoje na kuweka uwiano wa viwango vya safari kwenye mashirika mengine ya umma.
PAC pia imemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalumu katika matumizi tata ya Sh bilioni 26.
Matumizi hayo ni Sh bilioni 9.6 zilizotumika kwenye mkutano moja wa wafanyakazi, Sh bilioni 6.4 zilizotumika kwa ajili ya matangazo, Sh bilioni 10 zilizotumika kwenye safari na Sh bilioni 43 kwa ajili ya manunuzi ya dharura.
Kwa mujibu wa agizo la PAC, wafanyakazi hao watalazimika kulipa fedha hizo kuanzia mwaka 2011 hadi Januari Mosi, mwaka huu, yaani siku moja kabla Msajili wa Hazina hajatoa kibali kubariki posho mpya Januari 2 mwaka huu.
Menejimenti na Bodi ilipitisha viwango vya safari ambavyo ni Sh 500,000 kwa kada ya juu na Sh 125,000 kwa kada ya chini na ambavyo TPA walianza kuvitumia bila kupewa kibali tangu mwaka 2011 hadi Januari 1 mwaka huu. Viwango vya awali vilikuwa ni Sh 270,000 kwa ngazi ya juu na Sh 94,000 kwa kada ya chini.
“Ninawaagiza kuhakikisha wale wote walionufaika na viwango vipya vya safari kabla ya vibali kutolewa, kuhakikisha wanarudisha fedha hizo za umma, mtatafuta njia ya kuhakikisha wafanyakazi hao wanarejesha na hata kama ni kukatwa kwenye mishahara,” alisema.
Aidha, Zitto alisema: “ Nifikishieni salamu kwa (Lawrence) Mafuru (Msajili wa Hazina) kuhakikisha mnafanya ukaguzi wa haraka kwenye mashirika mengine kama Ewura, LAPF, NSSF na mengine kuangalia viwango vya safari wanavyolipana na ili kuweka usawa na kwenye mashirika.”
Aidha, Menejimenti ya TPA ililiambia Bunge kuwa watahakikisha mamlaka inatumia mfumo wa kisasa katika mahesabu na shughuli nyingine.
“Tulikuwa tunatumia mfumo wa kizamani ambao ulikuwa na matatizo lakini sasa tunataka kununua mfumo mpya wa ERP ambao pia hutumiwa na hata bandari za nchi zingine,” alisema Meneja wa Tehama, Phares Magesa.
Hatua hiyo ya kutaka kufungwa kwa mfumo wa kisasa wa kielektroniki katika hesabu na shughuli za bandari, unatokana na ripoti ya CAG kubainisha kutokuwapo kwa nyaraka zinazothibitisha matumizi kutokana na mahesabu kufanywa kwa mkono.
Katika ripoti hiyo, kwenye fedha zilizotumiwa kwa ajili ya mikutano ya wafanyakazi, zaidi ya Sh bilioni 600 hazina nyaraka ya matumizi yake na kwenye hoja ya matumizi ya matangazo Sh milioni 384 zimekosa nyaraka za matumizi yake.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande alisema uongozi wake umeweza kubadilisha sheria ambazo zilikuwa zikitoa mwanya kwa mkurugenzi kuidhinisha fedha zaidi ya bajeti na kwa kufanya hivyo, wameweza kupunguza matumizi kwa asilimia 30
No comments:
Post a Comment