Taarifa kutoka Mkoani Mwanza zinaeleza kuwa wale watoto mapacha waliozaliwa wakiwa wameungana katika eneo la kifua hadi tumboni, tukio lililovuta hisia za mamia ya wananchi waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara walikufa juzi katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Mapacha hao ambao ni wa kike walifariki dunia wakati madaktari wa hospitali hiyo wakijiandaa kuwafanyia upasuaji kwa ajili ya kuwatenganisha.
Mama mzazi wa watoto hao, Helena Paulo (20) ni mkazi wa Kata ya Buhare katika Manispaa ya Musoma Mara. Alifanikiwa kujifungua kwa njia ya upasuaji (operesheni) Januari 5, mwaka huu saa saba usiku.
Daktari katika Wodi ya Watoto ya Hospitali ya Rufaa ya Bugando Dk. Shukuru Kibwana, amesema walimpokea mama wa watoto hao Januari 5 na kwamba baada ya kuwafanyia uchuguzi wa kina watoto hao ilibainika kwamba wanaweza kutenganishwa kwa sababu kila mmoja alikuwa na mfumo wake unaojitegemea wa kula na kupata hewa hivyo kilichokuwa kimebaki ilikuwa ni matibabu upasuaji.
“Tangu tulipowapokea watoto hawa timu ya madaktari wa upasuaji na wataalamu wengine tulifanya kila lililowezekana kuokoa maisha ya watoto hawa lakini juhudi hizo hazikufanikiwa kama tulivyokuwa tunategemea kwa bahati mbaya waliaga dunia,” alisema Dk Kibwana.
No comments:
Post a Comment